Mafunzo kwa Wakulima juu ya udhibiti wa Sumukuvu kwa kutumia kiuatilifu cha Kibaiolojia “Aflasafe”

Mradi wa Kudhibiti Sumukuvu Nchini katika mpango kazi wake wa mwaka 2022/2023 ulipanga kutoa mafunzo kwa jumla ya wakulima 54,000 kutoka katika Halmashauri 18 za Tanzania Bara zinazotekeleza mradi ambazo ni Chemba, Kondoa, Babati, Itilima, Buchosa, Bukombe, Bahi, Urambo, Nzega, Kasulu, Kibondo, Kongwa, Kiteto, Kilosa, Gairo, Newala, Nanyumbu na Namtumbo. Mafunzo hayo yaliyoanza rasmi tarehe 5 Desemba, 2022 katika Halmashauri za Chemba, Kongwa, Urambo, Itilima, Newala na Kasulu na yataendelea katika Halmashauri zilizobaki ni mwendelezo wa mafunzo yaliyotolewa katika mwaka wa fedha 2021/2022 ( Aprili 2022- Mei 2022) ambapo wakulima walifundishwa kudhibiti sumukuvu katika mazao baada ya kuvuna. Katika awamu hii ya mafunzo, wakulima katika Halmashauri zote 18 watafundishwa na kusisitizwa kufuata kanuni bora za kilimo ili kudhibiti sumukuvu, msisitizo zaidi ukiwekwa katika matumizi ya kiuatilifu cha kibaiolojia kinachojulikana kama AFLASAFE kinachohusika moja kwa moja na kudhibiti uchafuzi wa sumukuvu, mazao yakiwa shambani.  Wataalam wanaohusika katika kutoa mafunzo hayo ni mabwana na mabibi shamba wa Halmashauri husika ambao walishapatiwa mafunzo ya udhibiti wa sumukuvu. Katika mafunzo haya, mashamba ya mfano ya wakulima katika kila Halmashauri yatatumika katika kutoa mafunzo na hivyo kuwapa fursa wakulima kufanya kwa vitendo waliyofundishwa.